SERIKALI
imewataka Watanzania kuacha kuweka vyakula vya moto katika mifuko ya
plasiti kutokana na uwepo wa uwezekano wa kupata magonjwa mbalimbali.
Taarifa
hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,
Mazingira, Stephen Masele wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalumu, Mkiwa Adam Kimwanga (CUF).
Katika
swali lake Kimwanga alitaka kauli ya Serikali kuhusu madhara ya
uwekaji wa chakula cha moto katika mifuko ya plastiki na kauli Serikali
kuhusu uchafuzi wa mazingira kutokana na kuzagaa kwa mifuko hiyo.
Masele
alisema kuweka chakula cha moto katika mifuko ya plastiki kunakuwepo
uwezekano wa kemikali zilizotumika kutengeneza mifuko hiyo kuingia
kwenye chakula na kukifanya kuwa sumu.
“Sumu
hii yaweza kusababisha saratani, kuharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi
hususan kwa watoto ambao bado kuzaliwa, mabadiliko ya kijenetiki,
matatizo ya kuona, uyeyushaji wa chakula tumboni kuwa taabu au
kutokamilika na ini kushindwa kufanya kazi,” alisema.
Alisema madhara mengine ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa utendaji wa figo na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa kupumulia.
“Ninawashauri
wananchi wasitumie mifuko ya plastiki na vifungushio vyake kuwekea na
kuhifadhia chakula kutokana na madhara yanayoweza kutokea,” alisema.
Aliwataka badala ya kutumia mifuko hiyo watumie vifungashio vya glasi, chuma isiyoshika kutu na vyombo vingine vya asili.
Alisema
pia Serikali inatambua uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya
plastiki na inachukua hatua mbalimbali ikiwemo kupiga marufuku matumizi
ya mifuko laini yenye unene wa chini ya maikroni 30 na kuhamasisha
matumizi ya mifuko mbadala.
Alisema
pia Serikali inafanya ukaguzi kwa makampuni, maduka na viwanda
vinavyozalisha na kusambaza mifuko ya plastiki nchini ili kujiridhisha
kama vinazingatia sheria.