Mama mjamzito anapaswa kutazwamwa kwa upekee sana wakati wote wa kipindi cha ujauzito ili kuweza kufahamu maendeleo na ukuaji wa mimba.

Moja ya mambo muhimu ya kuzingatia kwa mama mjamzito akiwa  katika hali hiyo ni pamoja na kuepuka kumeza madawa bila mpangilio au kupata ushauri kwa wataalam kwani kwa kufanya hivyo atakuwa akihatarisha maisha ya mtoto na yake pia.

Matumizi holela ya dawa wakati wa ujauzito huweza kuleta madhara kwa kupita kutoka kwenye damu ya mama na kuingia kwa mtoto kupitia kondo la uzazi. 

Baadhi ya dawa zinaweza kuleta madhara kwa mjamzito na hivyo kuathiri ukuaji wa mimba hiyo au kuathiri ukuaji wa mtoto moja kwa moja. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwa mwangalifu na dawa unazotumia wakati wa ujauzito.

Mfano mama mjamzito anapokuwa katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito,  hiki ni kipindi ambacho viungo mbalimbali huanza kutengenezwa, hivyo dawa pamoja na kemikali mbalimbali huweza kuathiri uumbaji wa viungo hivi na kuleta matatizo.

Yafuatayo ni madhara yanayoweza kutokea kwa mtoto endapo mama atakuwa akinywa dawa hovyo hovyo bila ushauri wa madaktari 
  • Kupata maumbile yasiyo kawaida, ambayo yanaweza kuathiri kichwa, ubongo, moyo, figo, miguu,mikono na viungo vingine vya mwili.
  • Kutokua vizuri
  • Mtoto kufariki akiwa tumboni
  • Mtoto kudumaa tumboni
  • Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo sana, njiti.
  • Mtoto kuzaliwa kabla ya wakati (premature birth)
  • Mimba kuharibika
  • Utindio wa ubongo
Hivyo kufuatia madhara hayo hapo juu, ni vyema mama mjamzito kuzingatia mambo haya yafuatayo kabla ya kuanza kutumia dawa:
  • Mama mjamzito unapokwenda hospitali tambua kuwa unawajibu wakumueleze daktari wako kuwa una ujauzito. Ni muhimu ajue ili usipewe dawa ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa mtoto wako.
  • Wakati wote wa ujauzito mama anapaswa kutumia dawa pale ambapo ugonjwa umethibitishwa na daktari na endapo ni muhimu sana kutumia dawa.
Hata hivyo, ni vyema ikafahamika kuwa ni muhimu sana kuwa makini na matumizi ya dawa na kemikali mbalimbali sio tu wakati wa ujauzito bali hata kabla ya ujauzito na kipindi chote unachotarajia kuwa na mimba na pale itakapo lazimu kutumia dawa wakati wa ujauzito, basi hakikisha umepata ushauri kwa daktari wako kuwa dawa ni salama na haitaleta madhara kwa mtoto tumboni mwako.
 
Top