Samaki ni kitoweo ambacho kinatajwa na kupendwa na watu wengi, kutokana na kuwa na ladha nzuri inayoweza kumfurahisha yoyote anayetumia kitoweo hiki. 

Samaki anasifika kwa kuwa na mafuta yenye kiambata aina ya 'Omega 3,' ambayo humfanya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na kutunza kumbukumbu vizuri pamoja na kuishi kwa muda mrefu.
 

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu kutokana na kutokuzeeka mapema. 

Mtaalam wa tiba asili Tabibu Abdallah Mandai, anasema endapo kitoweo hicho kitaliwa kwa wakati mwafaka yaani mara baada ya kuvuliwa huweza kuwa na tija zaidi kuliko kinapokaa. 


Tabibu Mandai anasema kuwa, 'Omega 3' husaidia katika ukuaji wa binadamu na kujenga ubongo wake vizuri, ndiyo maana watu wanaoishi katika maeneo yaliyozungukwa na maji mengi ‘bahari, mito au maziwa’ ni watu wenye akili nyingi na kwa wale ambao hawajaenda shule huwa waelewa zaidi na wakipelekwa shule hufanya vizuri zaidi katika masomo yao. 


Aidha, mtaalam huyo anabainisha kuwa kitoweo hiko ni msaada kwa kinamama wajawazito na mara nyingi wataalam wa afya huwashauri kinamama hao kutumia kitoweo hicho wawapo wajawazito na kuepuka nyama nyekundu. 


“Mama mjamzito anapokula kitoweo hiki husaidia sana kukuza ubongo wa mtoto,” alisema mtaalam. 
 
Mtaalam huyo anafafanua kuwa ‘Omega 3’ humsaidia mtoto kukuza ubongo, kutengeneza ‘retina’ kwenye mboni ya macho na kutengeneza mfumo wa neva.
 

Pia, humsaidia mama kuzuia matatizo ya kifafa cha mimba na sonono baada ya kujifungua na mara zote njia kuu ya mtoto hupata ‘Omega 3’ kutokana na vyakula anavyokula mama yake. 

Watoto ambao wamepata ‘Omega 3’ ya kutosha huonesha umakini mkubwa kuliko watoto wengine,huku wakielezwa kuwa watoto hao pia hukua kwa haraka zaidi kuliko yule ambaye hakupata kiambata hicho. 


Kwa wale watu wazima wao hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na saratani nyinginezo. Hivyo ni wazi kuwa ‘Omega 3’ inahitajika kwa kila binadamu ili kuendelea kuutunza ubongo na kujiepusha na magonjwa yanayotokana na kukosa madini haya. 


Wataalamu wanaelezea vyanzo vinavyoleta madini hayo kuwa vinapatikana katika samaki na mafuta ya samaki hasa samaki wenye mafuta mengi kama vibua, sato, salmon, sangara, dagaa, nk. 


Hata hivyo, unaweza kupata hii ‘omega 3’ kwenye juisi, mikate, mboga za majani, mayai, alizeti, mafuta ya samaki na vyakula jamii ya mbegu.
 
Top