Ajali za moto hutokea mara kwa mara, na huweza kumdhuru mtu yeyote bila kujali umri au jinsi. Mtu aliyeungua mara nyingi huitaji huduma ya kwanza wakati utaratibu wa kumuwahisha kwenye kituo cha afya ikiendelea. Usimkawize mgonjwa hospitali ili kutoa huduma ya kwanza!
Kuna vyanzo vingi vinavyoweza kumuunguza mtu vikiwemo;
- Vimiminika vya moto kama maji au mafuta
- Moto unaowaka
- Umeme
- Kemikali
- Mionzi
Mara nyingi watoto ndio huathirika sana na ajali hizi za moto. Mtu aliyeungua huitaji msaada wa haraka wa kitabibu kwani pamoja na kupata maumivu makali, hupoteza maji na madini mengi.
Huduma Ya Kwanza
Aina ya huduma ya kwanza utakayompa mtu aliyeungua itategemea na chanzo cha moto kilichomuunguza na ukubwa wa sehemu aliyoungua.
Unaweza kufanya yafuatayo kumsaidia aliye/anayeungua moto;
- Mwondoe kutoka kwenye chanzo cha moto. Kama bado anaungua au yupo karibu na moto, fanya jitihada kuuzima moto au kumuondoa kutoka sehemu yenye moto huo.
- Mweke mgonjwa vizuri, mtazame kama anapumua kwa kutazama kifua na tumbo. Kama hapumui mfanyie CPR.
- Mweke sehemu salama yenye hewa ya kutosha.
- Poza sehemu aliyoungua kwa kutumia maji safi yenye ubaridi wa kawaida kwa dakika 5 mpaka 10. Au tumia nguo safi uliyoilowesha kwenye maji safi kukanda sehemu iliyopungua. Kufanya hivi kunasaidia kupunguza joto na maumivu sehemu iliyoathiriwa. Kama ameungua sehemu kubwa, usikande au kuosha kwa maji.
- Mvue vitu vya kubana kama pete, mkanda, saa na vitu vingine kama vidani karibu na sehemu alizoungua. Wahi kabla hazijaanza kuvimba. Usiondoe nguo zilizogandia kwenye vidonda au kuungulia kwenye mwili.
- Usipasue malengelenge yaliyojitokeza baada ya kuungua
Inua sehemu aliyoungua juu zaidi ya usawa wa moyo. Kama ameungua kwenye miguu au mikono.
- Mfunike kwa nguo safi.
- Muwahishe kwenye kituo cha afya au hospitali iliyo karibu na wewe.