Mambo Ya Kutegemea Baada Ya Kujifungua


 
Kujifungua kwa njia ya kawaida kunaweza kuwa na kashi kashi kidogo, hasa maumivu ya uchungu. Baada ya kujifungua kwa njia ya kawaida, tegemea mambo yafuatayo, ingawa sio lazima upate yote.

Maumivu ya Sehemu za Siri

Mara nyingi sehemu za uke hupata michubuko na kuumia wakati wa kujifungua. Wakati mwingine njia inabidid iongezwe kwa kuchanwa. Hii huleta maumivu baada ya kujifungua ambayo hupungua kadri siku zinavyoenda.
Unaweza ukatumia dawa kwa ajili ya kupunguza maumivu kama paracetamol au diclofenac za kunywa au kupaka.
Kama unapata shida kwenye kukaa, tumia mto wakati wa kukaa.
Kama unapata maumivu wakati wa choo kikubwa, kula vyakula vyenye mboga za majani na mtunda kwa wingi. Pia unaweza kutumia dawa za kulainisha choo.

Damu Kutoka Ukeni

Damu huanza kutoka baada ya kujifungua na kuendelea kwa siku chache . Hujulikana kama lochia na rangi yake hubadilika kadri siku zinavyoenda. Siku chache za mwanzo huwa damu nyekundu na baada ya siku 4 -5 kubadilika kuwa majimaji zaidi yenye rangi ya kahawia. Kuanzia kwenyesiku ya 10 na kuendelea huwa na rangi ya njano njano. Maji maji haya hupungua kadri siku zinavyoenda na kuisha ndani ya wiki 6 baada ya kujifungua. Baadhi ya wanawake inaweza kutokea yakaendelea mpaka wiki ya 8.
Katika kipindi hiki kuwa makini kutazama kiasi cha damu kinachotoka, hasa pale unapobadilidha pamba au pedi ikiwa imeloa damu sana au maji yakiwa na harufu mbaya. Onana na daktari wako ikiwa hayo yanatokea.

Maumivu ya Tumbo

Siku chache baada ya kujifungua unaweza ukawa unapata mikazo na maumivu ya tumbo. Maumivu haya huitwa afterpains, hutokana na misuli ya tumbo la uzazi kusinyaa ili kuzuia damu nyingi kutoka. Huongezeka kadri idadi ya watoto uliojifungua na kupungu hasa baada ya siku ya tatu.  Unaweza kutumia dawa za maumivu kupunguza kama yanakuletea adhi.
Ikiwa unapata homa kali au tumbo linauma unapoligusa basi onana na daktari wako haraka.

Matatizo Wakati wa Kukojoa

Wakati wa kujifungua tishu za kibofu cha mkojo na njia ya mkojo huweza kuumizwa. Hii inaweza kuleta maumivu wakati wa kukojoa, lakini polepole yatapungua na kuacha. Mkojo unaweza kuwa unatoka wenyewe kidogo kidogo (leaking) hasa pale unapocheka au kukohoa. Hali hii huacha baada ya muda, tumia pedi na unaweza kufanya mazoezi ya Kegel ili kusaidia kuimarisha misuli ya sakafu ya kiuno.
Ukiona unapata maumivu makali ya kuungua wakati wa kukojoa, kukojoa kidogo kidogo mara nyingi sana onana na daktari.

Mabadiliko Katika Choo Kikubwa

Unaweza ukapata maumivu wakati wa kujisaidia choo kikubwa, kuhisi uvimbe au kutokwa na damu wakati wa kupata choo kikubwa. Kuvimba kwa mishipa ya damu kwenye mlango wa choo kikubwa (hemorrhoids) inaweza kujitokeza baada ya kujifungua. Kama unaogopa kujiumiza wakati wa kujisaidia, basi hakikisha unakunywa maji kwa wingi na kula vyakula vyenye kambakamba – mboga za majani na matunda. Unaweza kutumia dawa za kulainisha choo, osmotic laxative, hasa kama una hemorrhoids.
Ikitokea unashindwa kuzuia choo, onana na daktari wako. Unaweza kufanya mazoezi ya Kegel kusaidia kupunguza hali hii.
Wakati huu baada ya kujifungua ni muhimu kutunza na kuangalia afya yako na kumtunza mtoto wako.
 
Top