Wanawake wengi kwa kawaida huwa wanahisi uchovu wakati wa ujauzito. Uchovu, kulegea mwili na kuishiwa na nguvu ni jambo la kawaida katika kipindi hicho. Hii ni kwa sababu mwili katika kipindi hiki unatumia nguvu za kiada ili kuunda kiumbe kipya. Pia wakati huu mwili hutengeneza damu kwa wingi zaidi ili kufikisha chembechembe za chakula kwa mtoto, suala ambalo huufanya mwili ufanye kazi ya ziada na hata viungo vingine muhimu kama vile moyo na vinginevyo. Uzito wa mtoto nao unaoongezeka katika mwili wa mama mjamzito siku baada ya siku, ni sababu nyingine inayomfanya mama mjamzito ajihisi kuchoka. Kuchoka au kiushiwa na nguvu ni tatizo la kawaida hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya mimba. Katika miezi hiyo ya mwanzo ya mimba tatizo hilo husababishwa na mabadiliko ya homoni za mimba mwilini hasa progestrogen na wakati mwingine hali hiyo huongezwa na kichefuchefu na kutapika. Hali hiyo ya mchoko inatarajiwa kuisha inapoingia miezi mitatu ya pili ya mimba. Lakini pia kuna wengine ambao hali hiyo ya kuchoka huendelea nayo hadi wakati wa kujifungua. Kushindwa kulala vizuri kutokana na kwenda mara kwa mara msalani, au kukosa uzingizi kutokana na ongezeko la ukubwa wa tumbo mwishoni mwa ujauzito, ni miongoni mwa masuala ambayo humfanya mama mjazito ajisikie mchovu na akose nguvu siku nzima.
Vilevile mabadiliko ya kifizikia na kisaikolojia ya wakati wa ujauzito humfanya mama mjamzito awe na morali ya chini na kuhisi uchovu wa kimwili na hata kiakili. Sababu nyinginezo zinaweza kutokana na kazi mbalimbali anazofanya mama huyo au pia ukosefu wa lishe inayofaa na ya kutosha kwa ajili ya mwili wake, ambao unahitajia nguvu ya ziada hasa kwa ajili ya uumbaji wa ukamilifu wa mtoto aliye tumboni.
La muhimu analoshauriwa mama mjamzito ni kutoogopa na kutotishwa na hali hiyo, kwani inatokana na baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika mwili wake. La muhimu ni mama mjamzito kufuata ushauri unaotakiwa ili kukabilina na hali hiyo.
Zifuatazo ni njia za kukabiliana na uchovu wakati wa ujauzito.
• Kwanza kabisa mama mjamzito anatakiwa ale vyema. Mama mjamzito anatakiwa ale chakula bora na kamili, chenye kalori 300 au 500 za ziada ikilinganishwa na mtu asiye mjamzito kwa siku. Lakini awe mwangalifu na ni bora akigawe chakula chake katika sehemu ndogo ndogo 5 au 6 (suala hili tumelizunguzia kwa undani katika makala iliyopita ya kiungulia wakati wa ujauzito, tafadhali pitia makala hizo). Anaweza akawa akibeba matunda na mboga mboga kama asusa (snacks) kwa ajili ya kula kila anapohisi njaa popote pale awapo. Lakini ni bora ajiepushe na vyakula vyenye sukari nyingi na caffeine, kwani vyakula hivyo huyeyuka haraka mwilini na kumfanya ahisi njaa mapema.
• Mama mjamzito ahakikishe kuwa hana upungufu wa damu. Na kama anao basi atumie dawa za kuongeza damu zinazotolewa na madaktari, au ale vyakula vinavyoongeza damu. Hii ni kwa sababu ukosefu wa madini ya chuma mwilini unaosababisha ukosefu wa damu, ni miongoni mwa sababu zinazomfanya mama mjamzito ahisi kuchoka. Mtu mwenye ukosefu wa damu (Anemia) huhisi kubanwa na pumzi, ongezeko la mapigo ya moyo, udhaifu, kupauka na kizunguzungu. Onana na daktari iwapo una dalili kama hizo.
• Mama wajawazito wanashauri kujipumzisha nyakati za mchana. Ni bora mama mjamzito apumzike kwa kadri anavyoweza wakati wa mchana, baada ya chakula cha mchana au hata kabla ya nyakati za magharibi. Ikiwa unafanya kazi, basi pumzika mara kwa mara japo kwa muda mfupi ili kufanya mwili upate nguvu.
• Mama wajawazito wanashauriwa kujitahidi kulala mapema, hasa kama ikiwa inakubidi uamke mara kadhaa usiku kutokana na sababu mbalimbali, kama vile kwenda msalani, kula au kutokana na maumivu.
• Kufanya mzoeni husaidia kupunguza uchovu na kuna faida kemkem wakati wa ujauzito. Kahusiana na suala hilo soma makala zilizotangulia.
• Mama mjamzito anatakiwa anywe maji ya kutosha. Ukosefu wa maji mwilini huchangia kumfanya mama mjamzito ahisi uchovu.
• Usifanye kazi nyingi kutwa nzima, na kama inawezekana ni bora usaidiwe kazi hizo hasa za nyumbani na watu wengine katika familia kama vile watoto, mume ndugu, jamaa na marafiki.
• Usikilize mwili wako. Pale unaposikia njaa basi kula na pale unapojisikia uchovu jitahidi upumzike.
• Pata ushauri wa daktari iwapo unahisi uchovu wa kupindukia au unachoka kila mara, ili uwe na uhakika kuwa hakuna tatizo au hatari inayoweza kuhatarisha maisha yako na ya mtoto.