Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na kansa kwa wanaume duniani. Pia ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea. Hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata sana wanaume kuanzia miaka 25. Lakini kabla ya kuendelea mbele hebu kwanza tujue tezi dume ni zipi.
SARATANI NI NINI?
Saratani ni jina la gonjwa ambao hutokea wakati chembe chembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo. Kwa kawaida seli huwa zinajigawa, kupevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini seli za saratani hazifuati mfumo huo. Badala ya kufa, zenyewe huishi muda mrefu kuliko chembe chembe za kawaida na wakati huo huo huendelea kutengeneza seli nyingine na kuwa uvimbe wa saratani au tumour.
NINI KINATOKEA
Saratani ya tezi dume huwapata wanaume tu na hasa wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea. Kutokana na tafiti mbali mbali, saratani hii imethibitika kushika nafasi ya pili, ukiachia mbali saratani ya mapafu kwa kusababisha vifo vya wanaume wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea. Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS) na cha Afrika Kusini (CANSA) zimebaini kuwa, mwanaume mmoja kati ya sita hupata saratani ya tezi dume katika uhai wake. Kutokana na takwimu za mwaka 2010 za dunia nzima, malaria iliua watu laki tano, kifua kikuu watu milioni 2.1, Ukimwi watu milioni 1.8 na saratani watu milioni 9.9. Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani ni kubwa ikilinganishwa na ya magonjwa mengine. Dk Emmanuel Kandusi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa saratani hiyo, na mwanzilishi wa kampeni ya kuangamiza saratani ya tezi dume nchini Tanzania ya '50 Plus Campaign' anasema kuwa, ugonjwa huu ukitambuliwa mapema huweza kutibika kwa urahisi. Ameongeza kuwa, kutokana na ugonjwa huo kuwa hatari nchini humo, ifikapo mwaka 2020 unatarajiwa kuua watu milioni 20.
VIHATARISHI VINAVYOCHANGIA SARATANI YA TEZI DUME
· Umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.
· Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatarini ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi jeni za ugonjwa huo.
· Suala jingie ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama au (red meat) na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume.
· Vilevile wataalamu wanatumbia kuwa, wanaume wasiopenda kufanya mazoezi, wanene na wenye upungufu wa virutubisho vya Vitamin E pia wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo.
· Wanaume wengine walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na wale wenye asili ya Afrika (Weusi) ikilinganishwa na wazungu, wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali, wanaofanya kazi katika viwanda vya kutengeneza matairi na wachimbaji madini, hususan aina ya cadmium.
DALILI ZA SARATANI YA TEZI DUME NI ZIPI?
Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume au BPH. Dalili hizo ni pamoja na,
1) Kupata shida wakati wa kuanza kukojoa.
2) Kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa.
3) Kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu.
4) Kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku.
5) Kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote na
6) kutoa mkojo uliochanganyika na damu. Pamoja na kueleza dalili hizo wapenzi wasikilizaji wanapashwa kutambua kuwa, mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo, anapaswa kujua kuwa, seli za saratani katika tezi dume lake huwa zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea.
Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyigine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni. Aidha mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika.
USHAURI
Wanaume wanashauriwa kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya kibofu cha mkojo au prostate cancer kwa kuwa imegundulika kuwa wanaume wengi wakiziona na kuzihisi dalili hizo huona soni kwenda kumwona daktari na kufanyiwa uchunguzi. Baadhi ya watu huzihusisha na magonjwa ya zinaa au na dhana potofu za kishirikina. Wapo wanaokwenda mbali zaidi hata kuuita ugonjwa huo kuwa ni wa walawiti huku wengine wakiurahisisha kwa kuuita kuwa ni ugonjwa wa utu uzima kana kwamba saratani ya tezi dume ni jambo la kawaida kwa watu wazee. Mambo kama hayo hupelekea wanaume wengi kujinyanyapaa wenyewe na hata wengine kujitibu kwa uficho au kwa kutumia waganga wababaishaji mpaka pale mambo yanapokuwa yamewazidi ndipo hupelekwa mahospitalini na mara nyingine huwa wamechelewa na kupoteza maisha yao bure kwa ugonjwa ambao ungeweza kutibiwa mapema. Kwa ajili hiyo tunatoa wito kwa wanaume kutoona soni na kuwa na tabia ya kufanyiwa uchunguzi wa afya kwa ujumla, na hasa tezi dume angalau mara moja kwa mwaka.
Kuna vipimo viwili ambavyo daktari anaweza kumpima mwanaume ikiwa ni hatua ya kwanza ya kugundua ugonjwa huo. Vipimo hivyo vya kwanza ni "Digital Rectal Exam (DRE)" na cha pili ni "Prostate Specific Antigen (PSA)". DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume, lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au uvimbe katika tezi dume. Hivyo basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa. Baada ya vipimo hivyo kama vitaashiria saratani ya tezi dume basi daktari anaweza kuamuru vipimo vingine ili kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo kama vile transrectal ultrasound au prostatic needle biopsy. Tukumbuke kuwa kuwahi kugundua saratani mapema kabla ya dalili, kuna faida kubwa kwa muathirika kwani saratani ikigundulika mapema ni rahisi kutibika.
SARATANI YA TEZI DUME INATIBIKA?
Jibu ni ndiyo na kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa husika. Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi. Hii ni katika hali ambayo kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri mgonjwa kuwa chini ya uangalizi tu bila kufanyiwa upasuaji au bila kupatiwa tiba ya mionzi.
Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu au hormonal therapy, au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy). Naam wasikilizaji wapenzi hatuna la ziada kwa leo bali tukumbuke kuwa, saratani ya tezi dume ni ugonjwa wa kawaida kama yalivyo magonjwa mengine na uchunguzi na matibabu ya mapema huweza kuokoa maisha ya waathirika wengi wa ugonjwa huo. Basi hadi wiki ijayo panapo maajaaliwa, ahsanteni kwa kututegea sikio na kwaherini.