Kifafa cha mimba ni ugonjwa unaohusiana na msukumo mkubwa wa damu (high blood pressure) wakati wa ujauzito pamoja na kuharibika kwa viungo muhimu mwilini kama vile figo na ini. Kwa kawaida ugonjwa huu hutokea baada ya nusu ya kwanza ya ujauzito kuisha (kuanzia wiki ya 20 au miezi mitano ya ujauzito).
Ugonjwa huu huweza kuwatokea hata wajawazito ambao hawakuwa na tatizo la msukumo mkubwa wa damu kabla ya ujauzito.

Ugonjwa wa kifafa cha mimba unaweza kuleta madhara makubwa kwa mjamzito na mtoto aliye tumboni. Kuharibika kwa viungo muhimu kama figo na ini la mjamzito kunaweza kuwa kwa kiwango kikubwa kichoweza kusababisha mjamzito kupoteza maisha iwapo hatapata huduma ya afya mapema. Vilevile mtoto aliye tumboni anaweza kuathirika kwa kukosa damu ya kutosha toka kwa mama na kushindwa kukua vizuri na iwapo hali hiyo ikiendelea muda mrefu anaweza kufia tumboni.

Kutokana na hatari kubwa ya ugonjwa huu kwa wajawazito na watoto walio tumboni, inashauriwa kila mjamzito awe anahudhuria clinic na kupimwa msukumo wa damu (blood pressure) na mkojo ili kuhakikisha kuwa yuko salama. 
Iwapo kipimo cha msukumo wa damu ni kikubwa kuliko 140/90 mmHg, ni muhimu kurudia kipimo hicho baada ya muda na kufanya vipimo vingine vya maabara vinavyoweza kujulisha uwepo wa kifafa cha mimba.


Kwa kawaida ugonjwa huu huwepo kwa muda fulani bila mjamzito kuona dalili zozote. Ghafla mjamzito anaweza kuanza kuona dalili kama maumivu ya tumbo juu ya kitovu, kutapika, macho kutokuona vizuri, kuumwa kichwa, mkojo kuwa na rangi tofauti na kawaida, kupumua kwa shida, uchovu na maumivu ya viungo au kupoteza fahamu na “degedege“. 
Kila mjamzito mwenye dalili hizi ni muhimu aonwe na mtaalam wa afya ili apimwe na kupewa ushauri.


Sababu ya ugonjwa huu kutokea hazijulikani mpaka sasa ingawa zipo nadharia mbalimbali zinazojaribu kuelezea kutokea kwake. Mojawapo ya nadharia hizo inaelezea kuwa ugonjwa huu hutokana na matatizo ya ukuaji wa kondo la nyuma (placenta). Mishipa ya damu inayounda placenta ikikosea jinsi ya kujikita kwenye ukuta wa kifuko cha uzazi husababisha mishipa hiyo kuwa na tabia tofauti na ile ya kawaida na kusababisha mjazito kupata msukumo mkubwa wa damu na kifafa cha mimba. Kwa vile ugonjwa huu huonekana kutokea zaidi kwenye familia fulani kuliko nyingine, inaaminika kuwa urithi pia huchangia kupata ugonjwa huu. Hii inamaanisha mjamzito ambaye mama yake aliwahi kupata kifafa cha mimba ana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata kifafa cha mimba.

Wanawake ambao wana tatizo la msukumo wa damu, kisukari, unene kupita kiasi, ugonjwa wa figo kabla ya ujauzito wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata kifafa cha mimba. Kwa sababu hii, wanawake wote wenye matatizo haya wanashauriwa kufuatiliwa kwa karibu na mtaalam katika kipindi chote cha ujauzito.

Mjamzito aliyepata kifafa cha mimba kwenye ujauzito uliopita, ana uwezekano mkubwa wa kupata tena.
Imegundulika kuwa iwapo mwanamke anazaa na mwanaume mwingine tofauti na aliyezaa naye awali, uwezekano wa kupata kifafa cha mimba huongezeka.
Ujauzito kwa mwanamke mwenye umri zaidi ya miaka 40 huongeza uwezekano wa kupata kifafa cha mimba.

Ingawa hakuna kinga ya uhakika ya kifafa cha mimba, wanawake walio kwenye makundi hayo yaliyoyotajwa hapo juu kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huu wanaweza kujikinga kwa kutumia vidonge vya aspirin na madini ya calcium. Kabla ya kutumia dawa hizi ni muhimu kupata ushauri wa kitaalam.
Tiba pekee ya kifafa cha mimba ni kumzalisha mjamzito. Hii ni kwa sababu ugonjwa huu husababishwa na kuwepo kwa kondo la nyumba ndani ya kifuko cha uzazi. Bila kutoa kondo la nyuma mgonjwa hawezi kupona.

Iwapo ugonjwa huu utagundulika kabla mtoto hajakomaa na kuwa tayari kwa kuzalishwa. 
Daktari anaweza kushauri mjamzito alazwe na kuangaliwa kwa ukaribu wakati ikisubiriwa kukomaa kwa mtoto. Vilevile daktari anaweza kushauri mjamzito apewe dawa ya kuharakisha kukomaa mapafu ya mtoto.


Iwapo hali ya mjamzito ikibadilika na kuwa mbaya, kumzalisha huweza kuwa ni lazima hata kama mtoto hajakomaa kwa sababu kuna hatari kubwa ya mama na mtoto kuathirika iwapo ujauzito utaendelea. 
Mojawapo ya hatari inayoweza kutokea iwapo ujauzito utaachwa kendelea ni mtoto kufia tumboni, kupoteza fahamu kwa mjamzito na kupata dalili za “degedege“, damu kupoteza uwezo wa kuganda na kusababusha mjamzito kupoteza damu nyingi, damu kuganda mwilini na kuziba mishipa, kondo la nyuma kujitenga na kifuko cha uzazi kabla ya mtoto kuzaliwa, figo za mjamzito kushindwa kabisa kufanya kazi, mjamzito kupata kiharusi (stroke) au mjamzito kupoteza maisha.


Kwenye kumzalisha mama mwenye kifafa ch mimba njia mbalimbali huweza kutumika kutegemeana na hali ya mjamzito. Kama hali sio mbaya sana na njia ya uzazi imeshaanza kufunguka, mjamzito anaweza kupewa dawa za kuanzisha uchungu na kujifungua kwa njia ya kawaida. 
Kujifungua kwa njia ya operesheni hulazimika kwa wajawazito wenye msukumo mkubwa sana wa damu na wale ambao hali zao sio nzuri au kunapokuwepo na sababu nyingine ya kujifungua kwa operesheni.

Kabla ya kujifungua, mjamzito mwenye msukumo mkubwa wa damu hupewa dawa za kupunguza msukumo wa damu.
Ili kuzuia uwezekano wa kupata “degedege“, daktari anaweza kushauri mgonjwa apewe madini ya magnesium kwa njia ya dripu.


Kwa sababu ugonjwa wa kifafa cha mimba huongeza uwezekano wa damu kuganda mwilini, daktari anaweza kushauri mgonjwa atumie dawa ya kuzuia damu kuganda.
Baada ya kujifungua, msukumo wa damu unategemewa kurudi kwenye hali yake ya kawaida katika muda wa masaa 24. Hata hivyo ni vizuri mama aliyejifungua katika hali hii kuangaliwa kwa masaa 48 kabla hajaruhusiwa kwenda nyumbani. Hii hutegemea na uwepo na nafasi ya kulaza wagonjwa kwenye hospitali.

Kwa vile upo uwezekano wa msukumo wa damu kuendelea kuwa juu moja kwa moja. Mzazi hushauriwa kupima msukumo wa damu mara kwa mara, iwapo baada ya wiki sita (siku 40) itaonekana msukumo wa damu unaendelea kuwa juu, basi hushauriwa kuendelea na matibabu ya msukumo mkubwa wa damu kama wagonjwa wengine wenye ugonjwa wa msukumo mkubwa wa damu.
 
Top