Dalili 14 ZINAZOONESHA Kwamba Unatakiwa Umuone Daktari Wa Kinywa Na Meno Haraka
  1. Una Maumivu
Maumivu au uvimbe kwenye kinywa, usoni ama shingoni inaweza kumaanisha vitu kadhaa
Maumivu yanaweza kusababishwa na;
  1. Maumivu ya jino
Kama una maumivu kwenye taya au kinywa, jino linaweza kuwa sababu. Maumivu ya jino mara kwa mara huashiria tundu (yaani jino lililotoboka), ingawa wakati mwingine huashiria ugonjwa wa fizi. Vilevile maumivu ya jino huweza kuashiria jipu litokanalo na jino lililooza ama jino linaloota ambalo linakosa nafasi. Maumivu na hali hii inapaswa kutazamwa na daktari wa kinywa na meno mapema ili kujua tatizo halisi na sababu zake ili kuzuia jino husika kuoza na pia kumuondolea muhusika kero na usumbufu wa maumivu.
  1. Ganzi Ya Meno
Kama meno yako yanauma unapokunywa vitu vya moto au baridi,
inawezekana una ganzi ya meno. Hii inaweza kuwa imesababishwa na jino
kutoboka, jino kuvunjika, jino ambalo lilizibwa lakini limezibuka, jino
lililosagika,ama jino ambalo fizi zake zimejivuta kutokana na uwepo wa muda
mrefu wa ugonjwa wa fizi. Matibabu hutegemea chanzo cha hali hiyo. Kama
unahisi una hali kama hii Tafadhali muone daktari wa kinywa na meno ili upate
msaada haraka.
  1. Fizi Zilizovimba Na Kutoa Damu
Fizi Zilizovimba na/au kutoa damu huashiria ugonjwa wa fizi ambao ni rahisi sana kupona unapowahiwa kwenye hatua za awali. Kama fizi zako huwa na tabia ya kuvimba mara kwa mara na kutoa damu ni vizuri kumuona daktari wa kinywa na meno mapema ili kujua aina ya tatizo lako na matibabu yake
  1. Vidonda Kinywani
Kuna aina mbalimbali za vidonda vya kwenye kinywa ambavyo pia hutofautiana na visababishi vyake. Hali kadhalika vidonda kinywani huweza kuashiria maambukizi ya bakteria , fangasi ama virusi.
Vilevile vidonda hivi huweza kusababishwa na michubuko inayotokana na
kuvaa meno ya bandia, makosa katika uzibaji wa meno, ama meno
yaliyovunjika na hivyo kutengeneza ncha kali. Ni vizuri unapokuwa na hali ya
vidonda kwenye kinywa kumuona daktari wa meno ambaye ataangalia kidonda
husika na kutoa msaada unaostahili mapema.
   ZINGATIA: Kitaalamu ni lazima daktari wa kinywa akifanyie uchunguzi
kidonda chochote ambacho kimekaa kinywani zaidi ya wiki moja.
  1. Meno Yaliyopasuka Au Kuvunjika
Jino kuvunjika au kupasuka huweza kutokea kutokana na sababu mbalimbali
kama vile ajali. Mpasuko unaweza usionekane kwa macho na wakati mwingine
hata kwa mionzi, lakini huwa na maumivu makali wakati wa kutafunia ama
wakati ukifungua kinywa na hewa ikaingia kinywani. Ni vizuri kumuona daktari
wa kinywa na meno mapema ili kupata msaada unaostahili mapema
  1. Harufu Mbaya Ya Kinywa
Harufu mbaya inaweza kusababishwa na kutofanya usafi wa kinywa vizuri, mdomo kuwa mkavu, uvutaji wa sigara pamoja na magonjwa mengine. Hali ya harufu mbaya huwa ni dalili ya ugonjwa wa fizi. Kupiga mswaki mara mbili kwa siku na kufanya flosi ni muhimu katika kupunguza hali hiyo ya harufu mbaya kinywani na kuzuia ugonjwa wa fizi. Halikadhalika na kupiga mswaki ulimi huweza kusaidia. Ni vizuri kumuona daktari wa meno ili kufahamu zaidi juu ya chanzo na matibabu yake kama una tatizo hilo.
  1. Fizi Zako Zimevimba
Kama fizi zako zimevimba, zinatoa damu wakati unapiga mswaki au kuflosi au familia yenu ina historia ya ugonjwa wa fizi, ni wakati muafaka sasa kumuona daktari wa kinywa na meno ili apate nafasi ya kufanya uchunguzi juu yako.
  1. Unajaribu Kuficha Tabasamu Lako
Haijalishi kama unajistukia unapoona kuna jino au meno huna ama ungependa kuwa na tabasamu lililowazi na kujiamni zaidi katika hadhara ya watu, usijisikie vibaya ama aibu kumuona daktari wa kinywa na meno kwa msaada husika
  1. Kama Kuna matibabu Umefanyiwa
Ikiwa umeshawahi kufanyiwa matibabu yeyote ya meno kama vile kuzibwa ama unatumia meno ya bandia ni vizuri kuhakikisha unamuona daktari wa kinywa na meno mara kwa mara ili kuhakikisha hali yako ya meno na kinywa kiafya inakua nzuri muda wote
  1. Kama Una Magonjwa Sugu
Kama una magonjwa sugu kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, saratani, VVU/Ukimwi ni vizuri kumfanya daktari wa kinywa na meno kuwa sehemu ya timu inayo kuhudumia.Hii ni kwa sababu magonjwa hayo pamoja na madawa yake huweza kupelekea magonjwa ya kinywa
  1. Kama Ni Mjamzito
Ni sahihi na salama kwenda kwa daktari wa meno wakati wa ujauzito. Na ni ukweli usiopingika kwamba ujauzito unaweza kupelekea baadhi ya matatizo ya afya ya kinywa, hivyo unapaswa kumuona daktari mara kwa mara kwa faida ya afya yako ya kinywa.
  1. Una Matatizo Ya Kula
Shida wakati wa kufungua mdomo sio hali ya kawaida, shida wakati wa kutafunia sio hali ya kawaida, shida wakati wa kumeza chakula sio hali ya kawaida. Wakati haya yanatokea ni vema kumuona daktari wa kinywa na meno haraka na wakati huo kutumia vitu vya majimaji ili kupunguza maumivu.
  1. Una Kinywa Kikavu
Unapojihisi kuwa na kinywa kikavu inawezekana ni dalili ya ugonjwa Fulani sehemu fulani ya mwilini ama ni matokeo ya madawa ambayo huenda unayatumia. Hivyo ni muhimu kumuona daktari wa kinywa na meno mapema, hii ni kwa sababu kinywa kikavu pamoja na mambo mengine huweza kupelekea kutoboka kwa meno haraka.
  1. Unatumia Tumbaku
Kuanzia harufu mbaya ya kinywa mpaka saratani ya kinywa, vyote uvutaji wa sigara na matumizi ya ugoro ni hatari kwa afya ya kinywa na afya ya mwili mzima.
  1. Meno Yenye Madoa Au Rangi iliyofifia
Kadiri muda unavyokwenda meno huweza kubadilika rangi na kufifia. Hali hii huwa ni matokeo ya kula baadhi ya vyakula kama vile kahawa, chai, uvutaji wa sigara, matumizi ya ugoro na pariki, umri, ajali au hata baadhi ya madawa. Ni wakati wako muafaka wa kumuona daktari wa kinywa na meno ili kupata msaada husika.
  1. Taya Linauma
Kama taya lako linatoa sauti wakati wa kufungua na kufungua kinywa, ama unapata maumivu wakati wa kufungua na kufungua kinywa, au unapata maumivu ya taya wakati unatafuna , Vilevile kama unapata maumivu mara tu unapoamka ama unapokutanisha meno yako unahisi si yote yanayokutana ni muhimu na haraka kumuona daktari wa meno.
Kinywa Chako Kina Doa/Madoa au Vidonda
Kama kuna kitu hakikupendezi kinywani mwako ni vizuri kuzungumza na daktari wa kinywa na meno kwa ajili ya uchunguzi zaidi na ushauri.
Kuna aina mbalimbali za vidonda vya kwenye kinywa ambavyo pia hutofautiana na visababishi vyake. Hali kadhalika vidonda kinywani huweza kuashiria maambukizi ya bakteria, fangasi ama virusi
Vilevile vidonda hivi huweza kusababishwa na michubuko inayotokana na kuvaa meno ya bandia, makosa katika uzibaji wa meno, ama meno yaliyovunjika na hivyo kutengeneza ncha kali. Ni vizuri unapokuwa na hali ya vidonda kwenye kinywa kumuona daktari wa meno ambaye ataangalia kidonda husika na kutoa msaada unaostahili mapema.
ZINGATIA: Kitaalamu ni lazima daktari wa kinywa akifanyie uchunguzi kidonda chochote ambacho kimekaa kinywani zaidi ya wiki moja.
  1. Ni Wakati Wako Wa Kufanya Uchunguzi Wa Afya Ya Kinywa
Hata kama huna dalili ambazo zimeelezwa hapo juu, kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya ya kinywa na meno ni muhimu kwa sababu uchunguzi huo unaweza kupelekea kuzuia matatizo na pia kutibu dalili wakati bado changa na rahisi kutibika
 
Top