Miongoni mwa vitu vya msingi sana katika afya na maisha ya binadamu yeyote ni chakula bora na mlo kamili. Mlo kamili ndio msingi mkuu wa afya njema, kujengeka vizuri kwa mwili, kinga ya mwili na kupendeza kwa ngozi na nywele zetu. Mlo kamili ni mlo ambao una virutubisho aina zote katika kiasi sahihi kama inavyotakiwa na miili yetu. Mwili wowote utakaopatiwa chakula bora na milo kamili kama inavyotakiwa utapata faida zifuatazo:
- Utajengeka vizuri na kuendelea vizuri kila siku
- Utakuwa na kinga imara dhidi ya magonjwa na hautaumwa mara kwa mara
- Hautapata magonjwa yanayotokana na lishe mbaya au ulaji mbaya. Mifano ya magonjwa yanayoweza kusababisha na milo mibaya na ulaji mbaya ni kisukari, presha, uzito na unene mkubwa na uliopitiliza, kwashakoo, kiribatumbo, baadhi ya magonjwa ya moyo nk
- Hautapata magonjwa na matatizo mengine ya kiafya yatokanayo na upungufu wa vitamini na madini. Mifano ni beriberi, upungufu wa damu, matege, macho kushindwa kuona vizuri, matatizo ya uzazi, ngozi na nywele kuwa na afya duni nk
- Hautakuwa na ngozi na nywele zilizodhoofu, kukauka, kusinyaa, kuwahi kuzeeka nk
- Utawahi kupona magonjwa na vidonda vyote kila mara vitakapotokea
CHANGAMOTO YA KUPATA MLO KAMILI
Tuliwahi kujadili na baadhi ya watu katika jamii mbalimbali tunazopita kutoa elimu na ushauri wa afya na kupata baadhi ya majibu ya changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa chakula bora na mlo kamili. Baadhi ya changamoto zilikuwa ni za msingi na zingine hazikuwa za msingi bali ni kukosa uelewa wa mlo kamili unatakiwa uweje na kushindwa kupanga vyakula vyetu na milo yetu ili iwe milo kamili.
Changamoto ambazo jamii husema ni
- Kukosa uwezo wa kutosha kuweza kununua chakula bora na kutimiza mlo kamili
- Kukosa mbinu mbadala ya kuwezesha kupata vyakula vinavyotakiwa kwa ajili ya mlo kamili
- Kukosa uelewa wa mlo kamili unatakiwa uweje
- Kushindwa kupanga vyakula vyetu na milo ili iwe milo kamili
- Uhaba wa baadhi ya vyakula vinavyotakiwa katika mlo kamili kwenye baadhi ya mazingira
MLO KAMILI UNATAKIWA UWEJE?
Kimsingi mlo kamili ni rahisi sana kwa kuwa unamahitaji machache tu na mengi kati ya hayo ni vyakula hivi hivi tunavyokula kila siku. Changamoto kubwa sana katika hili ni kukosa uelewa wa mlo kamili unatakiwa uweje na kushindwa kupanga vyakula ili vitengeneze mlo kamili.
Kimsingi sahani ya mlo kamili inahitaji vitu vifuatavyo:
- Matunda na mboga za majani – Hivi vinatakiwa kuwa angalau nusu ya sahani (mlo) yako. Na ni kwa milo yote, asubuhi, mchana na jioni. Kula sana matunda na mboga za majani za aina na rangi mbalimbali
- Vyakula vya kukupa nguvu (wanga/carbohydrates) – Hivi vinatakiwa kuwa robo tu ya sahani yako. Mifano ni vyakula vinavyotokana na mahindi, mpunga, mtama, ngano nk. Tumia zaidi mbegu ambazo hazijakobolewa. Hizi zina virutubisho vingi zaidi na faida nyingi zaidi kuliko mbegu ambazo zimekobolewa tayari. Badala ya sembe kula dona. Badala ya mkate mweupe (White bread) kula mkate wa kahawia (Brown bread)
- Vyakula vya kukupa protini – Hivi vinatakiwa kuwa robo tu ya sahani yako. Tumia zaidi protini zinazotokana na mboga jamii ya maharage na mbegu zingine, kuku na samaki. Punguza kula nyama nyekundu kama vile ng’ombe na mbuzi.
Kuna ugumu wowote? HAKUNA!!!
Ni rahisi kama hivyo. Na vyote hivyo watu wengi wanavipata na kula. Kosa kubwa wanalofanya watu wengi ni kukosa mpangilio wa milo yao na kujikuta wakila zaidi vyakula vya aina moja na kuwa na upungufu au ukosefu wa vyakula vya aina nyingine.
Cha kuongezea hapo ni maji na mafuta ya kupikia.
Kunywa maji ya kutosha, angalau lita mbili kila siku. Kunywa kama maji au vinywaji vingine salama kwa afya yako kama vile juisi, chai, kahawa na maziwa; japokuwa unatakiwa usinywe sana maziwa na kahawa (Kikombe 1-2 kwa siku).
Tumia mafuta mazuri ya kupikia, salama kwa afya yako. Mfano ni mafuta ya mzaituni (Olive oil). Usitumie mafuta mengi, kijiko cha chakula kimoja hadi viwili yanatosha sana kwa chakula chako. Epuka kupikia mafuta yatokanayo na wanyama (Fats), epuka kupikia mafuta yanayokuwa kwenye hali ya kuganda.
Huo ndio mlo kamili. Na utakupatia virutubisho vyote, kinga imara dhidi ya magonjwa, mwili mzuri na ngozi na nywele nzuri. Kuna ugumu wowote?
Anza sasa. Fanya hivyo kwa milo yote na kila siku. Mlo wa asubuhi, mlo wa mchana na mlo wa usiku. Afya njema na muonekano mzuri unakusubiri…….