hedhi 2Maumivu wakati wa hedhi husababisha matatizo mengi kwa mwanamke kama vile kumyima raha na kumfanya ashindwe kuwa vizuri katika shughuli zake kama vile kazi, masomo, michezo na kadhalika. Huweza kuwa ya kawaida au makali, kuanza siku au masaa macheche kabla ya hedhi au wakati wa hedhi na huweza kuwepo kwa muda mfupi (masaa 12-72) au muda mrefu (zaidi ya masaa 72). Mara nyingi hutokea maeneo kama vile chini ya kituvu, sehemu ya chini ya mgongo, kwenye mapaja na nyonga. Ni muhimu kujua chanzo chake na jinsi ya kuyadhibiti ili kuweza kuishi bila wasiwasi wala shida hii. Pia ni muhimu kujua yanaashiria nini na kunaweza kuwa na tatizo gani jingine.
SABABU ZA MAUMIVU MAKALI
Sababu kuu ya maumivu haya ni kusinyaa kwa misuli katika tumbo la uzazi. Misuli hiyo ikisinyaa kwa nguvu huweza kusababisha mishipa ya damu kuziba kwa muda na hivyo kushindwa kufikisha hewa ya oksijeni (Hii tunayoivuta ndani wakati wa kupumua) kwenye baadhi ya maeneo ya mfumo wa uzazi na hivyo kupelekea maumivu, na ukali wa maumivu huongezeka kadiri misuli hiyo inavyozidi kusinyaa na kukaza.
AINA ZA MAUMIVU HAYA
Kuna aina mbili za maumivu haya na huashiria vitu tofauti
  1. Maumivu ya kawaida
Haya hutokea tu bila kuwa na sababu yoyote nyingine. Huwa ni ya muda mfupi (Masaa 12 hadi 72) na sio makali sana. Huwa yanapungua na kuisha kabisa yenyewe kadiri mwanamke anavyoongezeka umri au akijifungua mtoto
hedhi
  1. Maumivu yanayotokana na sababu zingine
Maumivu haya huja baada ya kuwa na tatizo jingine kwenye mfumo wa uzazi. Matatizo kama vile maambukizi ya magonjwa, uvimbe, uwepo wa vinyamanyama vidogo vidogo visivyo vya kawaida na vitu vingine vinavyoota kwenye tumbo la uzazi huweza kupelekea kuanza kwa maumivu haya.
Haya huwa makali zaidi na hudumu kwa muda mrefu kidogo (Zaidi ya masaa 72), na hupona kabisa baada ya chanzo husika kutibiwa/kuondolewa.
JINSI YA KUDHIBITI MAUMIVU HAYA
Unaweza ukapunguza maumivu haya kwa kuoga maji ya moto au kujiwekea chupa ya maji ya moto tumboni/chini ya kitovu na sehemu nyingine ambapo unahisi maumivu.
hedhi 3
Mazoezi ya mara kwa mara ya viungo pia husaidia kupunguza au kumaliza maumivu haya (Hususan maumivu ya kawaida).
Pumzika kwa muda na kunywa dawa za kutuliza maumivu.
hedhi 4
MATIBABU
Tatizo hili linatibika kabisa hospitali na utafurahia maisha yako kama kawaida. Cha msingi ni kufanyiwa uchunguzi na kujua ni nini haswa kinasababisha tatizo hili kwako na baada ya hapo kinatibiwa au kuondolewa na kisha maumivu yanaisha kabisa.
Unaweza ukapewa dawa za kutibu magonjwa au maambukizi ya bakteria kama chanzo ndo hicho au kusafishwa na kuondolewa vinyamanyama na vitu vingine vigeni vilivyojitokeza na kukua ndani ya sehemu za uzazi.
Utajisikiaje siku ambazo hautaumbuliwa na maumivu haya tena? Upo tayari kupata matibabu ya moja kwa moja na kuondokana na tatizo hili?
Usikae muda mrefu na tatizo hili, linaweza likawa ni ishara ya matatizo mengine yanayoweza kukusababishia matatizo makubwa zaidi kama vile kushindwa kupata mimba.
Nenda hospitali ukapate ushauri, vipimo na matibabu sasa. Inawezekana kabisa na ni rahisi sana.
Tunakutakia afya njema!
hedhi 1
 
Top