Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa macho mekundu (Red eyes) unaosababishwa na kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho ijulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” iliyoibuka nchini hivi karibuni.
.
Angalizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Prof. Pascal Ruggajo, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa awali ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kuathiri watu wengi nchini.
.
Prof.Ruggajo amesema dalili ya ugonjwa huo ni pamoja na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, kutoa machozi na kutoa tongo tongo za njano, ambapo amebainisha kuwa ugonjwa huo hauna tiba maalumu na kwamba hata bila ya kupata tiba dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili.
.
Aidha. Prof.Ruggajo amesisitiza wananchi kuzingatia usafi katika kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kutokana na tabia ya ugonjwa huo kusambaa kwa kasi, ambapo pia amewashauri wananchi kutokutumia dawa zisizo rasmi na ambazo hawajaandikiwa na daktari kwa wakati huo na kutotumia dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine ili kuepuka madhara.

 

 
Top