Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na
wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na
kumfanya apendeze na awe wa kuvutia.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa
hizo zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa
hizo ambazo huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.
Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata
alifanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina
kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa
na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma.
“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati
mwingine hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa
vichocheo aina ya estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa
fibroids,” anasema.
Dk Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi
hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla
hajakoma hedhi.
Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na
kujumuisha wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na
wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.
“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha
uvinbe kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za
kwenye mafuta ya ngozi kama vile mercury na hydroquionone,” anasema.
Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika
kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine
husababisha saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya
zebaki (mercury).
“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye
kwenye ngozi baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya
zenyewe kwenye ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” anasema.
Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi
kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama
zaidi kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza
vipodozi vyenye kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury,
vinyl chloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone,
steroids, methylene na chloroform.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk
Lauren Wise na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la
afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye
vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa
uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa
mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au
myoma.
Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa
za kulainisha nywele na kuangali umri walioanza kutumia dawa hizo, mara
ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi
gani.
Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za
kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146
waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi
na wengine kufanyiwa upasuaji.
Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise anasema mchanganyiko ulio kenye dawa za
nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati
makopo ya dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na
guanidine carbonate.
Bidhaa za kulainishwa nywele zilizoandikwa ‘no lye
relaxer’ zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha
na zile zilizoandikwa “Lye Relaxer”.
Uvimbe kwenye kizazi ni nini?
Ukuta wa nyumba ya uzazi umejengwa kwa misuli ya
tishu. Kwa kawaida uvimbe huu huanza kidogo kidogo na hukua hadi kufikia
ukubwa wa tikiti maji. Fibroids kubwa huweza kukua na kutanua nyumba ya
uzazi na kuwa sawa na ujauzito wa miezi sita au saba.
Mwanamke huweza kuwa na uvimbe mmoja mkubwa au vivimbe vingi ndani ya kizazi.
Daktari Bigwa wa magonjwa ya uzazi wa Kitengo cha
Upasuaji cha Chuo Kikuu Sayansi ya Tiba Muhimbili, Henry Mwakyoma
anauelezea fibroids ni uvimbe ambao upo katika umbile la misuli
myembamba na laini linalokua siku hadi siku.
“Sababu inayopewa kipaumbele zaidi ni wingi wa vichocheo vya estrogen ambavyo vipo katika miili ya wanawake,” anasema.
Dk Mwakyoma anafafanua kuwa, vichocheo hivi ndivyo
hufanya kazi katika mwili wa mwanamke na kumsababishia kupata siku zake
za hedhi.
“Ndiyo maana wengi wanaopata uvimbe huu, huwa ni
wanawake walio katika umri mkubwa au ambao tayari wamevunja ungo, kwani
ndiyo ambao huzalisha vichocheo vya estrogeni,” anabainisha mtaalamu
huyo.
“Dalili hutegemeana na eneo ulipokaa uvimbe na ukubwa wake.
Wengi hugundulika wakati wa kujifungua au endapo mwanamke atapata uvimbe
katikati ya kizazi, basi huweza kutokwa damu kwa wingi,” anasema.
Anaongeza: “Hata hivyo, asilimia 35 hadi 50 ya wanawake wanaougua maradhi haya huonyesha dalili wakati wa kujifungua,”
Dalili nyingine ni mwanamke kutokwa damu zake za
hedhi kwa wingi na kwa siku nyingi. Damu za hedhi huweza kuwa nyingi au
kidogo sana zikiambatana na maumivu makali.
Anasema wakati mwingine mwanamke huweza kuhisi ana ujauzito kwani uvimbe huu huwa mkubwa na huchezacheza kana kwamba ni kiumbe.
“Nina mifano hai, wapo wanawake waliowahi kuhisi
wana ujauzito, wakakosa kabisa siku zao za hedhi, wakaona dalili zote za
mimba na kumbe walikuwa na uvimbe wa fibroids,” anasema.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza anasema wamekuwa wakifanya ukaguzi mara kwa mara kuzuia uuzwaji wake.
Isitoshe akasema: “Elimu inatolewa kwa wananchi
pia ili kuwafahamisha kuhusu madhara ya vipodozi hivyo kwa sababu
wanunuzi wasipokuwepo basi hata biashara haitakuwepo.”
Pamoja na hayo, adhabu hutolewa ya kuwanyang’anya na kuwapeleka mahakamani wenye maduka makubwa wakiziuza.
Credit: Mwananchi