
Zifuatazo ni faida anazozipata mama mjamzito iwapo atafanya mazoezi
1. Mazoezi hupunguza maumivu ya kichwa, kukosa choo na kuvimba mwili.
2. Mazoezi huongeza nguvu na kuupa mwili stamina.
3. Mazoezi hukufanya ujisikie vizuri na kukufanya uwe katika hali ya furaha.
4. Mazoezi hupunguza maumivu ya mgongo na huimarisha mifupa ya mgongo, makalio na mapaja na kuifanya iwe na uwezo wa kuvumulia vyema uzito wa mimba.
5. Mazoezi husaidia huongeza mtiririko wa damu na hewa katika ngozi na kuifanya ngozi yako ionekane nzuri.
6. Mazoezi hutayarisha mwili wako uwe tayari kwa ajili ya kuhisi uchungu kwa muda mfupi na kujifungua kwa urahisi.
7. Mazoezi hufanya mwili wako urudi upesi katika muonekano wake wa kawaida baada ya kujifungua.
8. Mazoezi humsaidia mama mjamzito apate usingizi kwa wepesi na kulala vyema.
Hata hivyo mama majamzito anashauriwa kabla ya kuanza kufanya mazoezi apate ushauri wa daktari na kuhakikisha kuwa hana matatizo ambayo kwa kufanya mazoezi pengine yakahatarisha mimba yake. Kwa wale waliokuwa wakifanya mazoezi kabla ya kubeba mimba wanashauriwa kuendelea na mazoezi yao lakini kwa kuwa waangalifu na kwa kiwango kidogo. Lakini kwa wale ambao walikuwa hawafanyi mazoezi hawaruhusiwi kufanya aina zote za mazoezi wakati wa ujauzito. Mazoezi kama vile kuogelea (kwa wale anaojua kuogelea), kutembea na yoga ni miongoni mwa mazoezi yanayoshauriwa wakati wa ujauzito. La muhimu ni mama mjamzito kutokaa tu na kujiepusha na uvivu na pengine kwa kufanya shughuli zake tu za kawaida ambazo mama huwa anazifanya nyumbani kila siku ikawa inatosha kuwa mazoezi yake na akaongeza kwa kutembea kidogo ( walking) kila jioni. Kutembea ni mazoezi salama na rahisi kwa kila mama mjamzito na yanayojulikana na kila mtu na kuweza kufanywa mahala popote. Ni bora kama unaweza fanya mazoezi na mwenza wako, rafiki au hata ndugu na jamaa yako ili uweze kufurahia zaidi mazoezi hayo. La muhimu ni kufuata maelekezo ya daktari kwani si kila mama mjamzito anaruhusiwa kufanya mazoezi wakati wa ujauzito kutokana na sababu tofauti. Baadhi ya mazoezi ambayo yana madhara kwa afya ya mama mjamzito na kwa mtoto hayaruhusiwi kabisa kufanywa wakati wa ujauzito. Mazoezi hayo ni kama vile mazoezi ya aerobic, ski, kupanda mawe, kupanda farasi na mengineyo kama hayo. Iwapo unaishi katika miji iliyoendelea basi unaweza kupata kwa urahisi vituo maalum kwa ajili ya kufanyia mazoezi mama wajawazito, na katika vituo hivyo kwa kawaida wakina mama wajawazito hukusanyika na kufanya mazoezi kwa pamoja. Lakini kama uko katika miji ambayo vituo hivyo hakuna usife moyo, na jitahidi kufanya mazoezi hayo peke yako huku ukishirikiana na familia yako.
Makala hii inaendelea...