Kipindi cha ujauzito ni kipindi muhimu sana kwa mama. Kwa kina mama wengi kipindi hiki kinakuja na majukumu mengi na changamoto za kiafya. Mara nyingi matatizo ya kiafya wakati wa ujauzito yanatokana na mabadiliko ya homoni mwilini mwa mama mjamzito. Na sio ugonjwa unaohitaji matibabu. Hata hivyo usafi wa kinywa pia unapaswa kuangaliwa na kupewa kipaumbele. Kuna usemi kwa kina mama wajawazito kuwa kila ujauzito huondoka/hupelekea kuongoa jino, au kuwa na maumivu ya meno. Na ni ukweli usiopingika kuwa matatizo ya meno kuoza huwa ni tatizo sugu linalochukua muda mrefu, na pengine limekuwepo hata kabla ya uzauzito. Ni vyema mama mjamzito akawasiliana na daktari wa afya ya kinywa kufanya uchunguzi wa kinywa ne meno pia kwa ushauri zaidi.
 Matibabu ya meno wakati wa ujauzito
Kwa wajawazito wengi, matibabu ya kinywa na meno ni salama, ni vyema kumweleza daktari wa afya ya kinywa juu ya umri wa mimba. Mama mjamzito amweleze daktari juu ya dawa zozote anazotumia na kama ana ushauri wowote amepewa na daktari mwingine katika kliniki nyingine alizohudhuria (kama kliniki ya mama wajawazito). Kama mama mjamzito ana mimba hatarishi au matatizo mengine ya kiafya, dakari wa afya ya kinywa anaweza kuwasiliana na daktari wa binadamu (physician) au daktari bingwa wa afya wa kinamama (obstetrician) au kupendekeza matibabu kuahirishwa.
Namna ambavyo ujauzito unaaweza kuathiri afya ya kinywa cha mama mjamzito
Japokuwa wanawake wengi wanaweza kufika miezi tisa bila tatizo la afya ya kinywa, ujauzito unaweza kusababisha baadhi ya matatizo ya afya ya kinywa kuwa mabaya zaidi, au kujenga matatizo mapya. Uangalizi wa afya ya kinywa mara kwa mara na tabia njema kwa afya ya kinywa na meno unaweza kumsaidia mama mjamzito na mtoto wake wawe na afya njema.
Mabadiliko yanayotokea kinywani wakati wa ujauzito
  1. Kupata ugonjwa wa fizi unaosababishwa na ujauzito
Mdomo wa mama mjamzito unaweza kuathirika na mabadiliko ya homoni wakati wa ujauzito. Kwa mfano, baadhi ya wanawake hutokewa na hali inayojulikana kama "ugonjwa wa fizi utokanao na ujauzito”, (pregnancy gingivitis). Ugonjwa huu husababisha fizi kuwa nyekundu, kuvimba na kuuma. Fizi pia zinaweza kutoa damu kidogo wakati wa kupiga mswaki au zinaposafishwa na uzi maalumu unaoitwa “dental floss”. Tatizo hili halina uhusiano na uchafu unaosababisha ugonjwa wa fizi unaojitokeza kwenye meno (dental plaque). Mara nyingi ukichunguza kinywa cha mama mjamzito mwenye tatizo hili, utakuta ana usafi wa kuridhisha sana wa meno yake. Tatizo hili likiachwa bila kutibiwa, linaweza kusababisha aina mbaya zaidi ya ugonjwa wa fizi, ambao husababisha ufizi kulika, meno kulegea, na hata kungooka. Ni vyema mama mjamzito akamwona daktari wa afya ya kinywa na meno kwa ushauri zaidi.
  1. Kuongezeka kwa Hatari ya kuoza kwa meno
Wanawake wajawazito wanaweza kukabiliwa zaidi na uwezekana wa meno kutoboka (kuoza) kwa sababu kadhaa. Kama vile kuongezeka tabia ya kula vitu vya sukari kama pipi, biskuti n.k. Ugonjwa kutapika asubuhi kwa wajawazito (Morning Sickness) unaweza kuongeza kiasi cha asidi mdomoni, ambayo huweza kuaribu mwonekano wa nje wa jino yako (dental erosion).
Wakati wa ujauzito upigaji wa mswaki (mara mbili kwa siku), na utumiaji wa uzi wa kusafisha katikati ya meno (dental floss), unaweza kupungua sana, hii hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kutapika asubuhi (morning sickness), hali ya kutaka kutapika kitu chochote kinapoingia mdomoni (sensitive gag reflex), maumivu ya fizi, na uchovu wa kupitiliza (exhaustion).
Ni muhimu hasa kwa mama mjamzito kujitahidi kufuata kawaida yake ya usafi wa kinywa, maana usafi usioridhisha wa kinywa (poor oral hygiene) wakati wa ujauzito umekuwa umehusishwa na watoto kuzaliwa njiti (premature delivery), na uzito mdogo (low birth weight), ukuaji usioridhisha wa mtoto kwenye nyumba ya uzaji (intrauterine growth restriction), kisukari wakati wa ujauzito (gestational diabetes na dalili za kifafa cha mimba (pre-eclampsia).
  1. Uvimbe kwenye fizi wakati wa ujauzito (pregnancy tumors)
Baadhi ya wanawake, wanapata uvimbe kwenye sehemu ya ufizi unaoitwa “uvimbe wa fizi utokanao na ujauzito" (pregnancy tumors). Hali hii hujitokeza kwenye ufizi, mara nyingi wakati wa miezi mitatu ya pili ya ujauzito (second trimester).
Hii sio kansa lakini ni uvimbe tu ambao hutokea mara nyingi kwenye ufizi kati ya meno wakati wa ujauzito. Pia unaweza kuhusiana kuongezeka kupita kiasi kwa uchagu au utando kwenye meno ujulikanao kitaalamu kama “dental plaque”. Hii hupelekea kwa fizi hutoa damu kwa urahisi na kuwa nyekundu. Kwa kawaida tatizo hili hutoweka baada ya mtoto kuzaliwa. Inashauriwa mama mjamzito mwenye tatizo hili apate ushauri kutoka kwa daktari wa afya ya kinywa.
Chakula muhimu wakati wa ujauzito
Je, unajua kwamba meno ya mtoto wako yanaanza kuumbika kati ya miezi tatu mpaka sita toka ujauzito umetunga? Hivyo virutubisho vya kutosha vinavyosaidia utengenezaji wa meno ya mtoto vinahitajika; hasa vitamin A, C, na D, na protini, na madini ya kalsiamu na fosforasi.
Ni jambo la kawaida kwa mwanamke mjamzito kuwa na hamu ya kula zaidi, na kula mara kwa mara. Tabia hii inaweza kumsababishia kuoza kwa meno.

Ni vizuri kuchagua vyakula visivyo na sukari ila viwe na lishe kwa ajili ya mama na mtoto wake kama vile matunda na mbogamboga, mtindi, na kuhakikisha anafuata ushauri wa daktari wake kuhusu chakula. 









Vipimo vya mionzi (dental x-ray) ni salama
Picha ya eksirei ya meno (dental x-ray) wakati mwingine ni muhimu wakati wa matibabu ya meno kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo la dharura linalosumbua kwenye meno. Wakati wa kupiga eksirei, mpigaji atatumia aproni maalumu yenye uwezo wa kuzuia mionzi, hivyo kumlinda mama na mtoto wasipatwe na mionzi isiyohitajika, hasa kwenye mfuko wa uzazi.
Ugonjwa wa kutapika asubuhi wakati wa ujauzito

 Kama mama mjamzito anasumbuliwa na hali ya kutapika mara kwa mara hasa wakati wa asubuhi, ajaribu kusukutua na maji yaliyochanganywa na unga wa baking soda kijiko kidogo, hii itasaidia kuzuia asidi kutoka tumboni (wakati wa kutapika) kushambulia meno yake.
Matumizi ya madawa wakati wa ujauzito
Ni vyema mama mjamzito amjulisha daktari wake wa afya ya kinywa na meno juu ya dawa zozote anazotumia hata kama hazihusiani na tatizo la afya ya kinywa.
Habari hii itamsaidia daktari wake wa afya ya kinywa kuamua ni aina gani ya dawa, iwapo atahitaji kumwandikia. Pia daktari wake wa afya ya kinywa anaweza kushauriana na daktari mwingine (physician/obstretician) ili kuchagua dawa kama vile dawa za kutuliza maumivu au antibiotics itakayokuwa salama wakati wa ujauzito. Madaktari wote wanajali afya ya mama mjamzito na mtoto wake, hivyo asisite kuwauliza chochote kuhusu dawa wanayopendekeza.
Matumizi ya dawa ya ganzi ya mdomoni wakati wa ujauzito
Tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya dawa ya ganzi ya mdomoni kwa kina mama wajawazito ni salama kabisa kwake na kwa mtoto wake. Hivyo matibabu kama kuziba meno, kutibu mzizi wa jino, kung’oa jino n.k yanaweza kufanyika bila shida wakati wa ujauzito.
Baada ya mtoto kuzaliwa
Utunzaji wa afya ya kinywa unapaswa kuwa endelevu hata baada ya kujifungua. Pia linaongezeka jukumu la kutunza afya ya kinywa ya mtoto. Ingawa watoto wachanga kawaida hawana meno, wengi wao huanza kuota meno wastani wa miezi sita baada ya kuzaliwa. Inashauriwa kuanza kusafisha kinywa cha mtoto katika siku chache za kwanza baada ya kuzaliwa kwa kuufuta ufizi na na kitambaa safi, chenye unyevu. Meno yanapoanza kuota mdomoni muda wowote huweza kuoza kama hayatatunzwa vizuri.
 
Top