Kila ifikapo Septemba 29, kila mwaka duniani kote huazimishwa siku ya moyo, siku hii hulenga kutoa fura kwa watu wote duniani kujilinda na magonjwa ya moyo na mishipa ya moyo ambayo huchangia vifo vingi.

Inaelezwa kuwa ifikapo mwaka 2030 zaidi ya watu milioni ishirini na tano watakuwa wamepoteza maisha kutokana na maradhi haya ya moyo hususani katika nchi zenye uchumu wa kati.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku hii ya magonjwa ya moyo daktari bingwa Tulizo Shemu kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete amesema magonjwa ya moyo huchangia kwa asilimia 31 ya vifo vyote vinavyosababisha takribani watu milioni 17.3 kufa kila mwaka.

Dk Shem ametaja baadhi ya sababu ambazo huchangia magonjwa ya moyo, ambazo ni pamoja na matumizi ya tumbaku, chumvi, vyakula vyenye mafuta, pombe na kutofanya mazoezi.

Sababu nyingine ni pamoja na unene uliokithiri, kutotibu ugonjwa wa kisukari na kuwa na mafuta mengi kwenye damu.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo kuweka mazingira mazuri ya afya bora ya moyo katika sehemu zetu tunazofanyia kazi kwa kuhakikisha kila mtu anatoa mchango katika kujenga afya bora ya moyo ili kupunguza visababishi vinavyochochea magonjwa hayo.
 
Top